BENKI YA EXIM YAZINDUA MASHINE YAKE YA KWANZA YA KUWEKA PESA KWENYE AKAUNTI

indexMkuu wa  Huduma za matawi Benki ya Exim Tanzania, Bw Eugine Massawe (kulia) pamoja na Meneja Mkuu wa kampuni ya Pacific International Lines, PIL Bw. Kevin Stone wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya kuweka pesa (CDM) ya benki hiyo itakayowawezesha wateja wa kampuni ya PIL kuweka pesa kwenye akaunti zao moja kwa moja bila kulazimika kufika kwenye ofisi au kuhudumiwa na wafanyakazi wa benki hiyo.

……………………………………………………………………………………………………………

Na Mwandishi wetu

BENKI ya Exim Tanzania imezindua mashine yake ya kwanza ya kuweka pesa (CDM) itakayowawezesha wateja wa kampuni ya Pacific International Lines, PIL kuweka pesa kwenye akaunti zao moja kwa moja bila kulazimika kufika kwenye ofisi au kuhudumiwa na wafanyakazi wa benki hiyo.

Ufunguzi wa mashine hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ukihusisha mwakilishi wa benki hiyo ambaye ni Mkuu wa  Huduma za matawi Bw Eugine Massawe pamoja na Meneja Mkuu wa kampuni ya PIL Bw. Kevin Stone.

Akizungumzia mashine hiyo iliyopo kwenye jengo la Maktaba (Makataba Square)lililopo katikati ya jiji, Bw Massawe alisema ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kurahisisha huduma zaidi za kifedha kwa wateja wa benki hiyo.

“Mashine hii itawawezesha wateja wetu kuweka pesa moja kwa moja kwenye akaunti zao wao wenyewe. Huduma hii itapatikana kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 na nusu jioni kila siku na itatoa fursa kwa wateja         wa PIL kupata msaada kutoka kwa wahudumu wetu waliopo jirani na mashine pale watakapohitaji,’’ alisema

Kwa mujibu wa Bw Massawe, kwa kuanzia mashine hiyo itaanza kupokea noti za Dola ya Kimarekani kwa kiasi chochote huku akitahadharisha; “Ifahamike kwamba mashine hii ina uwezo mkubwa wa kutambua pesa bandia au zile zisizofaa kwa kuwa imewekewa mfumo bora kabisa wa kiusalama,”

Aliongeza kuwa mashine hiyo inamuwezesha mtumiaji  kupata risiti ya muhamala atakaoufanya sambamba na kumuhakikishia mafanikio ya muhamala husika.

“Mteja atapokea ujumbe mfupi wa maneno kuhusiana na mwenendo ya muhamala alioufanya,’’ alisema Bw Massawe huku akisisitiza: “Benki ya Exim itabaki kuwa benki pekee yenye kubuni huduma zinazokidhi matakwa ya wateja kulingana na mabadiliko ya kimahitaji katika huduma za kibenki,’’

Alisema huduma hiyo imewekwa jirani na makao makuu ya benki hiyo ili kuwawezesha watumiaji wa huduma hiyo kupata msaada kwa urahisi kutoka kwa wafanyakazi wa benki pale wanapohitaji.

“Itakapofikia kipindi ambacho wateja wetu watakuwa tayari wamejenga uelewa wa kutosha kuhusiana na matumizi sahihi ya mashine hii tutakuwa tayari kuongeza mashine nyingine katika maeneo mbalimbali ili waweze kufurahia huduma hii zaidi,’’ aliahidi.

About

Hello, I am a regular author. To edit this text edit your profile in Users area of admin.