“SI KWELI KABISA”: HAKUNA KODI YA NG’OMBE NCHINI

Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi imekanusha kodi ya ng’ombe iliyoripotiwa na Umoja wa wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao yake wa Wilaya ya Kinondoni.

Taarifa hii imetolewa na Katibu Mkuu (Mifugo) wa Wizara hiyo Dkt. Mary Mashingo baada ya kuyaona malalamiko ya wafanyabiashara hao kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini.

Katika taarifa hiyo wizara imekanusha kuwa kodi ya ng’ombe siyo shilingi 18,500 kama ilivyoripotiwa na wafanyabiashara hao bali ni shilingi 12,000 ambayo inatambulika kisheria.

“Wizara yetu inapenda kutoa ufafanuzi juu ya kodi inayotozwa katika machinjio ya Kimara kama ifuatavyo: ushuru wa soko shilingi 5000, ushuru wa kusafirisha mifugo shilingi 1500, ushuru wa ukaguzi wa wanyama shilingi 2500 pamoja na gharama za machinjio shilingi 3000 kwa kila  kichwa cha ng’ombe ambapo jumla yake ni shilingi 12,000”alisema Dkt.Mashingo.

Aidha,taarifa  hiyo imeelezea kuhusu kupitisha ng’ombe katika soko la upili la Pugu kabla ya kuwapeleka katika machinjio ya Kimara kuwa ni kwa ajili ya kuwafanyia vipimo vya afya ng’ombe hao kabla ya kuchinjwa pamoja na kulipia tozo ya Serikali.

Taarifa hiyo pia imefafanua baadhi ya sababu za kufungwa kwa machinjio ya Kimara tangu Aprili 9 mwaka huu zikiwemo za baadhi ya wafanyabiashara kupeleka ng’ombe katika machinjio hayo moja kwa moja bila kupitia Pugu ambalo ni kosa kisheria pamoja na uchafu uliokithiri katika machinjio hayo.

Katika kufanya juhudi za kupambana na matatizo haya,Wizara  ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inajipanga kukutana na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake ili kuwaelimisha zaidi kuhusu Sheria, Kanuni, na Taratibu zinazopaswa kufuatwa katika ufanyaji wa biashara hii.

About

Hello, I am a regular author. To edit this text edit your profile in Users area of admin.